Hukumu Inaanzia katika Nyumba ya Mungu

Derek Prince
Published: 1993
Last Updated: October 2026
Read Time: 8
This teaching is not currently available in ខ្មែរ.
Hukumu ya Mungu huanza na watu wake, ambao wanawajibika kwa kweli waliyoipokea. Maandiko yanaonya dhidi ya kupenda mali na kulegeza msimamo, kisha yanawaita waamini wajinyenyekeze kwa kuungama. Kuungama kwa kweli kwa Mungu na kwa wengine huondoa kiburi na kuandaa njia kwa ajili ya maombi yenye nguvu.
Kama Wakristo wa Marekani, tunakabiliwa na ukweli mgumu, usiopingika: taifa letu limekuwa chini ya hukumu ya Mungu. Kuna sababu nyingi za hali hii, lakini zote zinaweza kufupishwa kwa kauli moja rahisi: Tumefanya dhambi ambayo Esau alikataliwa - tumeidharau haki yetu ya mzaliwa wa kwanza ( Waebrania 12:15-17 ).
Uchambuzi huu unahusu hasa hali ya Marekani. Hata hivyo, mengi ninayoyasema yanahusu pia mataifa mengine ambayo yamerithi urithi wa imani ya Kiyahudi na Kikristo, pamoja na Kanisa ulimwenguni kote. Mungu na atusaidie kila mmoja wetu kukubali wajibu wake binafsi!
Mungu anatuhukumu kulingana na kipimo cha nuru tulichopokea. Yesu aliwaambia Wayahudi wa siku zake kwamba hukumu yao ingekuwa kali zaidi kuliko ile ya Sodoma na Gomora, kwa sababu walikuwa wamepokea ufunuo mkubwa zaidi wa ile kweli ( Mathayo 11:20-24 )
Hali hiyohiyo inaihusu Marekani katika karne hii. Hakuna taifa jingine ambalo limepata fursa kubwa ya kulifikia Neno la Mungu kama ile waliyopewa watu wa Marekani. Kupitia utamaduni na desturi, makanisa na wainjilisti, redio na televisheni, pamoja na machapisho mbalimbali, Marekani imebarikiwa kuliko mataifa mengine yote kwa kupata maarifa ya kweli ya Mungu. Kwa hiyo, hukumu yetu kwa kuikataa kweli hiyo itakuwa kali zaidi. Wakristo wengi hawatambui kwamba hukumu ya Mungu haianzi kwa watu wa ulimwengu, bali kwa watu wa Mungu. Petro aliwaambia Wakristo wa siku zake:
“Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? ( 1 Petro 4:17 )
Maneno haya yanahusu pia Kanisa la Marekani leo. Miongoni mwa dhambi zote ambazo Kanisa la sasa linaweza kulaumiwa kwa kuzitenda, inatosha kuangazia mbili: kupenda mali na kulegeza msimamo kuhusu kweli ya Mungu. Katika Luka 17:26–30, Yesu alitabiri kwamba kipindi kitakachotangulia kurudi kwake kingefanana na siku za Nuhu na Lutu. Alitaja hasa shughuli nane zilizokuwa za kawaida katika siku hizo: kula, kunywa, kuoa, kuolewa, kununua, kuuza, kujenga na kupanda. Hata hivyo, hakuna shughuli yoyote kati ya hizi ambayo yenyewe ni dhambi. Basi, tatizo lilikuwa nini?
Tatizo lilikuwa kupenda mali. Watu wa siku hizo walikuwa wamejishughulisha sana na mambo ya kimwili kiasi kwamba hawakutambua hukumu ya Mungu iliyokuwa inakaribia juu ya maisha yao yaliyotawaliwa na tamaa za mwili. Hukumu ilipofika, hawakuwa wamejiandaa kabisa. Hali ni hiyohiyo leo kwa watu wengi nchini Marekani wanaodai kuwa Wakristo. Ikiwa hukumu za mwisho za Mungu zingeanza ghafla na kuleta kurudi kwa Kristo, hawangekuwa wamejiandaa kabisa.
Kama ilivyo kwa kupenda mali, dhambi ya kulegeza msimamo kuhusu kweli ya Mungu mara nyingi haitambuliwi. Miaka kadhaa iliyopita, nilipokuwa nikiomba, niliona katika akili yangu picha ya sehemu ya ndani ya jengo la kawaida la kanisa, lenye safu za viti, jukwaa, mimbari, piano na vitu vingine. Lakini jengo lote lilikuwa limejaa ukungu wa aina fulani. Maumbo ya vitu yangeweza kutambulika, lakini hakuna kitu kilichoonekana waziwazi. Nilipokuwa nikijiuliza ukungu huo uliwakilisha nini, Mungu alinipa neno moja lililo wazi: kulegeza msimamo.
Katika Kanisa la sasa, kweli nyingi muhimu zinazohusu maadili na mafundisho ya imani, ambazo zimeelezwa kwa uwazi kabisa katika Agano Jipya, zimepoteza uwazi na nguvu yake. Katika 1 Wakorintho 6:9–10, Paulo aliandika:
“Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyanganyi hawataurithi ufalme wa Mungu..”
Hata hivyo, leo Kanisa limejaa watu wanaotenda dhambi hizi bila kuwa na wasiwasi wowote. Kwa kweli, mara nyingi hata hujivunia dhambi hizo.
Mshiriki mmoja wa kanisa alikuwa amelazwa hospitalini, akiwa katika hali ya kufa kutokana na UKIMWI alioupata kupitia vitendo vya ushoga. Kisha akampokea Kristo na kupewa Agano Jipya. Baada ya kusoma sehemu fulani ya Agano Jipya, alituma ujumbe wa haraka kwa mtu aliyemwongoza kumpokea Kristo: “Njoo uniombee. Ninahitaji kufunguliwa. Sikujua kamwe kwamba kulikuwa na jambo lolote lisilo sahihi katika mtindo wangu wa maisha.”
Miaka kadhaa iliyopita, wakati wa msimu wa Krismasi, wafanyakazi wetu walikuwa wamefanya mipango ili mimi na Ruth tushiriki katika vipindi viwili vya televisheni kwenye mtandao wa PTL. Kwa kuwa sisi hatutazami televisheni, hatukujua tungetarajia nini. Nilipaswa kuwa “mnenaji mkuu.” Katika saa ya kwanza, nilipewa dakika kumi, na katika saa ya pili, nilipewa dakika ishirini. Muda mwingi ulitumika kuomba michango ya fedha na kuuza wanasesere wa Tammy. Kwa kadiri ninavyokumbuka, mimi na Ruth ndio pekee tuliomtaja Yesu.
Muda mfupi baadaye, kashfa ambazo sasa zimejulikana sana zilifichuliwa hadharani. Lakini kwangu binafsi, jambo lililonishtua zaidi halikuwa makosa ya kingono au ya kifedha, ingawa yalikuwa mazito sana. Kilichonishtua wakati huo, na kinachoendelea kunishtua hadi leo, ni kutambua kwamba mamilioni ya Wamarekani walikuwa wakionyeshwa mara kwa mara picha potofu kabisa ya Ukristo—Ukristo ambao haukuwa na nafasi kwa msalaba na matakwa yake ya unyenyekevu, utakatifu na maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine. Inasikitisha sana kutambua kwamba watu waliodanganywa na namna hiyo ya kuwasilisha Ukristo huenda wasipate kamwe kuisikia kweli halisi ya Injili!
Kashfa ya huduma ya PTL sasa imekuwa sehemu ya historia, lakini imetuachia swali ambalo tunahitaji kulijibu: Je, lilikuwa tukio la pekee lisilohusiana na mengine, au lilikuwa dalili ya ugonjwa unaouathiri Mwili wa Kristo kote Marekani?
Hata hivyo ndani ya kanisa bado kuna masalia ya wafuasi waaminifu na waliojitolea wa Yesu. Ikiwa sisi ni miongoni mwa idadi hiyo, ni jinsi gani Mungu anatuhitaji tukabiliane na majanga ya sasa?
Jibu moja la wazi linapatikana katika 2 Mambo ya Nyakati 7:14:
ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekeza na kuomba na kuutafuta uso wangu, na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao, na nitaiponya nchi yao.
Maneno, "Watu wangu wanaoitwa kwa jina Langu" kinatumika kwa Wakristo wote wanaojichukulia jina la Kristo.
Kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifundisha kuhusu andiko hili, lakini hivi karibuni nilikabiliwa na ufahamu ulionishtua sana! Watu wa Mungu katika siku zetu hawajawahi kutimiza sharti la kwanza. Hatujawahi kujinyenyekeza kwa kweli. Kiburi chetu—cha kidini na cha kibaguzi kwa misingi ya rangi—bado ni kizuizi kinachozuia majibu ya maombi yetu kwa ajili yetu wenyewe na taifa letu.
Kupitia jinsi Mungu alivyoshughulika nami kwa ukali katika maisha yangu mwenyewe, nimejifunza njia yenye matokeo zaidi ya kujinyenyekeza. Kwa ufupi, njia hiyo ni kuungama dhambi zetu. Ikiwa tunaungama dhambi zetu mbele za Mungu mara kwa mara na kwa unyoofu, haiwezekani kumkaribia tukiwa na mtazamo wa kiburi. Zaidi ya hayo, nimegundua kwamba Mungu ameahidi kutusamehe dhambi tunazoziungama tu.
“Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutokana na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)
Dhambi ambazo hazijaungamwa ni dhambi ambazo hazijasamehewa. Hivyo, kizuizi cha kiburi hujenga kizuizi kingine cha dhambi ambazo hazijasamehewa.
Biblia inatuhimiza kuungama dhambi zetu si kwa Mungu pekee, bali pia kwa sisi kwa sisi.
“Kwa hiyo, ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana ili mpate kuponywa.” (Yakobo 5:16)
Kuungama dhambi zetu kwa Mungu hushughulikia kiburi kinachoathiri uhusiano wetu na Mungu, ilhali kuungama dhambi zetu sisi kwa sisi hushughulikia kiburi kinachoathiri mahusiano yetu na watu wengine. Ni vigumu kuendelea kuwa na mtazamo wa kiburi kwa mtu ambaye tumemwungamia dhambi zetu binafsi muda mfupi uliopita.
Jambo hili linahusu hasa uhusiano kati ya waume na wake. Wale wanaoungamiana dhambi zao mara kwa mara hawatenganishwi na kizuizi cha kiburi.
Zaidi ya hayo, kuungama dhambi ni sharti muhimu la msingi kwa ajili ya maombi yenye matokeo ya kuwaombea wengine. Danieli alikuwa mmoja wa watu wenye haki zaidi katika Biblia, lakini alipoanza kuwaombea watu wake wa Israeli, alianza kwa kukiri kwamba yeye mwenyewe pia alikuwa na sehemu katika dhambi zao (Danieli 9:3–13).
Ninaamini kwamba Mungu anatungoja sisi Wakristo wa Marekani tujinyenyekeze mbele zake na mbele ya wengine kwa kuungama dhambi zetu. Ni baada tu ya kufanya hivyo ndipo tunapoweza kuendelea kudai ahadi yake ya kuiponya nchi yetu. Lakini ni lazima nitoe neno la tahadhari. Msijishughulishe na kujichunguza kupita kiasi hadi mkajikuta mnajilaumu na kuhuzunika isivyofaa! Roho Mtakatifu ni “kidole cha Mungu” (Mathayo 12:28; Luka 11:20). Mwombeni Mungu aweke kidole chake juu ya dhambi mnazohitaji kuziungama. Atafanya hivyo kwa usahihi usiokosea, na huenda akazifunua dhambi ambazo hamkuwahi hata kutambua!

ទាញយកដោយឥតគិតថ្លៃ
សេចក្តីបង្រៀននេះអាចទាញយក បោះពុម្ព និងចែករំលែកសម្រាប់ការប្រើប្រាស់ផ្ទាល់ខ្លួន ឬក្នុងព្រះវិហារ។
ទាញយក PDFកូដ: TL-L001-100-SWH
