Praying for the Government - Part 1

Derek Prince
*Last Updated: Mei 2026
16 min read
This teaching is not currently available in Kiswahili.
Kwa ujumla, unaweza kusema kwamba Wakristo wanapata serikali wanayostahili. Inachukua muda. Haifanyiki papo hapo. Lakini kwa jumla, Wakristo wanawajibika kwa serikali inayowatawala. Ikiwa ungetumia wakati mchache kukosoa na wakati zaidi wa kuomba, utakuwa na machache ya kukosoa.
Kuna njia mbali mbali ambazo kanisa linaweza kufanya mamlaka yake yawe na matokeo ulimwenguni. Ningependekeza njia nne: sala, kushuhudia, kuhubiri, na kufanya matendo mazuri. Hizi ndizo njia za msingi ambazo Mungu anatarajia kanisa kutumia ushawishi wake.
Mungu anatamani kanisa liwe na nguvu ya kutawala katika mambo ya ulimwengu huu kupitia maombi. Hii imeonyeshwa wazi katika maandiko. Ikiwa kanisa linashindwa kufanya hivi, kanisa limekuwa chumvi ambayo imepoteza ladha.
Katika 2 Mambo ya Nyakati 7:14 tunasoma: "Ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekeza na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao. ” Huu ni ufunuo uliotolewa na Bwana kwa Sulemani baada ya kuweka wakfu hekalu. Wengine wana mtazamo kwamba: Ahadi hiyo alisema kwa Sulemani zamani sana katika Agano la Kale na haina maana kubwa kwetu leo. Nitauzungumzia mtazamo huu kwa kifupi.
Katika 2 Wakorintho 1:20 tunasoma: "Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni "Ndiyo." Kwa sababu hii ni kwake yeye tunasema "Amen” kwa utukufu wa Mungu. ” Sio ahadi kadhaa - lakini ahadi zote! Sio zilikuwa, sio zitakuwa - lakini ni ndiyo! Si tu Ndiyo, lakini kama bado una mashaka, ni Ndiyo na Amina! ndani yake [Kristo] kwa utukufu wa Mungu kupitia kwetu sisi. "Sisi" inamaanisha Wakristo wote, wewe na mimi tukijumuishwa. Je! Tunamtukuzaje Mungu? Kwa kunena kwa dhati ahadi Zake! Kadri tunavyo nena kwa dhati ahadi za Mungu, ndivyo tunavyomtukuza Mungu. Ahadi zote za Mungu zinapatikana kwa ajili yetu katika Kristo leo.
Kurejelea ahadi kwenye 2 Mambo ya Nyakati 7:14, naamini unaweza kuona jinsi ahadi hii inatuhusu, wewe na mimi leo! Mungu anasema “Ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu,” Ikiwa wewe ni Mkristo, hiyo inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba jina la Kristo limehusishwa nawewe. Unahusishwa najinala Kristo. Unatambuliwa kama Mkristo kwa jina la Kristo. Kwa hivyo ahadi hii inatumika kwa Wakristo: watu wa Mungu ambao jina la Kristo limehusishwa.
Mungu anasema ikiwa watu wake watafanya mambo manne, atafanya mambo matatu. Watu wa Mungu lazima wafanye mambo manne kwanza, kabla Mungu hajafanya mambo matatu ambayo ameazimia kufanya. Ni ahadi yenye masharti. Mungu hasemi kwamba atafanya bila masharti, lakini anasema, "Ikiwa watu Wangu watatimiza masharti Yangu, basi nitafanya mambo haya."
Kuangalia mwisho wa aya ile, jambo la mwisho ambalo Mungu atawafanyia watu wake ni kuponya nchi yao. Ni wazi kuwa hii ndio nchi wanamoishi. Mungu anasema kwamba kufanya vitu ambavyo vitasababisha Mungu kuponya nchi wanamoishi kupo ndani ya uwezo wa watu wake. Tazama nchi tunayoishi. Inahitaji uponyaji? Kuna jibu moja tu. Ndio! Ukweli kwamba nchi inahitaji uponyaji inaonyesha kwamba watu wa Mungu wameshindwa kufanya kile Mungu aliwaambia wanapaswa kufanya. Wajibu ni wetu sisi - sio wa yule mtu anayetumia madawa ya kulevya, sio wa huyo kahaba. Wajibu ni kwa watu ambao wameitwa kwa jina la Kristo!
Ikiwa nchi yetu haijaponywa, kuna sababu moja tu. Hatujafanya mambo ambayo Mungu anahitaji. Ninaamini kuwa hii ni kweli. Ni njia nyingine tu ya kusema kile Yesu alisema katika Mathayo 5:13: “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu." Ikiwa nchi yetu haijaponywa na uwepo wetu, basi chumvi yetu imepoteza ladha.
Chumvi hufanya nini? Kwanza kabisa, inatia ladha. Maadamu tupo ulimwenguni, tunaupa ulimwengu ladha mbele ya Mungu. Kwa maneno mengine, Mungu anapokea ulimwengu kwa sababu ya Wakristo. Mungu anaendelea kuonyesha ulimwengu neema na rehema badala ya ghadhabu na hukumu, kwa sababu ya uwepo wetu.
Naamini kwamba kuna tofauti mahali ambapo mimi nipo. Niligundua hili wakati wa Vita vya pili vya dunia. Askari wengine walikuwa salama nilipokuwepo. Askari wasiomwamini Kristo walijua hili. Wakati tulipokuwa kwenye hali ngumu katika jangwa la Afrika Kaskazini, baadhi ya wanajeshi hao waliokufuru walinigeukia na kuniambia, “Koplo Prince, nimefurahi kuwa uko pamoja nasi.” Je! Elisha alimwambia nini Eliya? “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” (2 Wafalme 2:12). Walikuwa wapi? Sio karibu na wafalme lakini karibu na manabii.
Sisi ndio ulinzi wa nchi. Sisi ndio ngome ya taifa lolote. Fikiria mfano wa Sodoma. Abrahamu akamwambia Mungu, “Ikiwa kuna watu kumi wenye haki, je! Utaokoa mji?” Mungu akasema, “Ndio." Lakini hakuweza kuuokoa mji kwa sababu hakuweza kupata watu kumi wenye haki. Sijui idadi ya watu huko Sodoma, lakini najua kuwa kiwango hicho hicho bado kinatumika. Watu kumi wenye haki wanaweza kuokoa mji wenye ukubwa wa Sodoma. Watu mia wenye haki wanaweza kuokoa mji mara kumi ukubwa wa Sodoma. Wanaume elfu moja wanaweza kuokoa mji mara mia ukubwa wa Sodoma. Na kadhalika. Naisikitikia dunia hii wakati kanisa litakapoondoka. Hakutakuwa na chumvi tena. Kisha ghadhabu na hukumu zitamiminika bila kizuizi chochote. Lakini tunapokuwa hapa, sisi ni chumvi ya dunia.
Chumvi pia huhifadhi. Inazuia uharibifu. Katika siku kabla ya jokofu, nyama ilihifadhiwa na chumvi. Ilizuia uharibifu. Tuko hapa kwa nini? Ili kuzuia uharibifu. Uharibifu wa kila aina- wa maadili, kijamii, kisiasa. Kadiri sisi tuko hapa, tunafanya hivi. Yesu alisema, “Ikiwa chumvi imepoteza ladha yake, itawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Basi haifai chochote ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. "Wakati kanisa litaacha kutekeleza kazi yake kama chumvi, litatupwa nje na kukanyagwa chini ya miguu ya wanadamu. Watu hawa wanaweza kuwa wakomunisti au Wanazi au wafuasi wa itikadi nyingine ambayo bado haijatokea. Lakini itakuwa ni watu ambao watakanyaga kanisa ambalo halitimizi jukumu lake ulimwenguni kama chumvi.
Je! Ni mambo gani ambayo Mungu anataka watu wake wafanye? Kwanza kabisa, “Watu wangu watajinyenyekeza.” Hilo ndilo jambo gumu sana kwa watu wa dini. Sisemi hivyo kwa utani, namaanisha kwa dhati. Unasikia watu wengine wakisema, "Mungu, nifanye mimi kuwa mnyenyekevu.”Mungu hakuwahi kusema hivyo. Mungu alisema, "Jinyenyekeze.” Hakusema, "Nitakufanyia." Mungu hawezi kukunyenyekeza. Mungu anaweza kulazimika kukudhalilisha, lakini pekee mtu anayeweza kukunyenyekeza ni wewe mwenyewe. Unyenyekevu lazima utoke kwa kitendo cha ndani cha mapenzi yako. Hauwezi kuja kwa njia nyingine yoyote. Usipoamua kujinyenyekeza, unaweza kufedheheshwa lakini bado unajivuna kama tausi.
Sharti la kwanza ni kujinyenyekeza na kumtii Mungu. Ikiwa tutamtii Mungu, pia tutalitii Neno Lake na mamlaka Yake. Ni rahisi kusema kwamba tunamtii Mungu, lakini Neno la Mungu linasema: Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi.......Ninyi wake, watiini waume.....Enyi watoto, watiini wazazi wenu” (Waefeso 5: 21-22; 6: 1). Hapo sio rahisi sana. Watu wengi wanadai, “nimemtii Mungu,” lakini wakati mtihani unakuja katika uhusiano wao na watu wengine, ni wazi kuwa sio watiifu.
Ikiwa utajinyenyekeza, lazima uwe mtendaji. Sio jambo mbaya wakati mwingine kupiga magoti mbele za Mungu. Je Umewahi kufanya hivyo? Sema, "Mungu, mimi niko hapa na ndipo nastahili kuwa! Mimi ni mnyoo. Nilitoka kwa mavumbi na mavumbini ndio nafasi yangu. “Je! Unafikiri huu ni ushabiki tu bila kufikiri? Soma biblia na uone idadi ya watu ambao walienda mbele za Mungu: Abrahamu, Musa, Daudi, Danieli. Hakuna mtakatifu mashuhuri wa Mungu ambaye hakuandikwa kwamba alienda mbele za Mungu. Ikiwa palikuwa mahali pazuri kwa Musa, Daudi, Danieli na wengine, sidhani kama itakuwa chini ya hadhi yako.
“Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekeza.” Hii ni hatua ya kwanza na huwezi kuiacha. Mungu ana mpango wake wa Kiroho uliopangwa katika daraja: daraja la 1, daraja la 2, daraja la 3, daraja la 4.Hadi utakapopita daraja la 1, hautawahi kwenda daraja la 2. Haijalishi ikiwa utarudia daraja la 1 miaka kumi, Mungu hatakukuza. Ndio maana wengine wamekwama kwa muda mrefu katika daraja moja. Usifikirie, “Bwana, sikuweza kufanya vyema daraja la 1, lakini nitafanya vizuri katika daraja la 2. Niruhusu nipite hili na nitafanya linalofuata." Hapana, haiwezekani hivyo!
Hatua ya pili ni kuomba. “Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekeza, na kuomba." Usianze kuomba hadi ujinyenyekeze. Unyenyekevu huja kabla ya maombi.
"Omba na utafute uso Wangu.” Hatua ya tatu ni kutafuta uso wa Mungu. Je! Hiyo inamaanisha nini? Ninaelewa inamaanisha kuingia moja kwa moja mbele ya Mungu Mwenyezi - ambapo kila kizuizi huondolewa, na unakuja uso kwa uso na Mungu Mwenyezi. Unaweza kuwa na mkutano wa maombi, lakini sio kumaanisha ni kutafuta uso wa Mungu.
Kijana mmoja alikuja kwangu akitafuta ubatizo wa Roho Mtakatifu. Alikuwa mfanyakazi wa vijana kanisani. Nilimwambia ningemuona Jumatano jioni. Alisema ilibidi ahudhurie mkutano wa maombi jioni hiyo. Nikasema, “Nadhani hiyo haitakuwa nzuri.” “Ah, hapana," alisema, “hiyo itakuwa sawa. Tunaomba kutoka saa mbili hadi saa tatu. “Huo ni mkutano wa maombi, lakini sio kutafuta uso wa Mungu. Unapotafuta uso wa Mungu, hauachi hadi uingie kwenye uwepo wa Mungu-hata ikiwa inachukua usiku kucha. Kuna maombi mengi ambayo hayatafuti uso wa Mungu. Yanakoma tu kwa kuwasiliana na Mungu.
Hatua ya nne: "wageuke kutoka kwa njia zao mbaya." Nani? Walevi, vijana ambao hawaendi kanisani? Hapana, Wakristo - watu wa Mungu! Kizuizi cha uamsho kipo ndani ya kanisa, sio nje. Hakijawahi kuwa nje.
Je! Unajua hukumu inaanza wapi? Kwenye nyumba ya Mungu. “Kwa kuwa wakati umefika,” Petro anasema, “Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu” (1 Petro 4:17). Ili kuifanya iwe wazi kabisa, anaongeza, "Basi kama ikianzia kwetu sisi." Kisha anauliza, "mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?" Mungu siku zote hufanya kazi hivi. Anaanza na watu wanaojua zaidi. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi. (Luka 12:48). Unasema, “Ndugu Prince, sina uovu wowote.” Ninajibu, “Hujamkaribia Mungu vizuri kuweza kuona. Ikiwa ungeingia kwenye uwepo wa Mungu, ungeona njia zako mbaya. Unaposema hauna uovu unaonyesha ni jinsi gani ulivyo mbali na Mungu. "
Baada ya hatua hizi nne, Mungu anasema, "Nitasikia kutoka mbinguni.” Mungu hajaahidi kusikia kila sala. Je! Ulijua hivyo? Ninauhakika kwamba katika makanisa mengi sala haziendi zaidi ya dari. Mungu hajaahidi kusikia kila sala. Kwa kweli, Mungu anasema, Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba. (1 Yohana 5:15). Ugumu sio kumfanya Mungu ajibu, lakini kumfanya Mungu asikie.
"Basi, nitasikia kutoka mbinguni, na nitawasamehe dhambi zao." Dhambi za nani? Dhambi za kahaba au mtumia dawa za kulevya? Hapana, dhambi ya kanisa!
"Nitaiponya nchi yao.” Kwangu suala hilo ni wazi. Ikiwa nchi haijapona, kosa ni kwa watu wa Mungu. Nimezingatia hili, nimeliombea, na nimetafakari juu yake. Wajibu wa hali ya Afrika upo kwenye mlango wa kanisa. Ninaamini kuwa hili ni kweli. Ikiwa nchi yetu haijapona, jukumu lipo kwetu. Ninashiriki jukumu hilo na wewe. Sikwambii kitu ambacho ni kweli juu yako lakini si juu yangu.
Uponyaji Kupitia Μαομβι
Tunawezaje kuleta uponyaji? Nitazungumza nawe juu ya maombi. Msingi wa mafundisho yangu unatoka katika mistari nne ya kwanza ya 1 Timotheo sura ya 2:
- 1. Awali Ya Yote, Nasihi Kwamba Dua, Sala, Maombezi na Shukrani Zifanyike Kwa Ajili Ya Watu Wote:
- Kwa ajili ya wafalme na wote walio katika mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.
- Jambo Hili Ni Jema, Tena Linapendeza Machoni Pa Mungu Mwokozi Wetu,
- Anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli.
Let us consider these words.
Paulo anasema, Awali ya yote, omba!" Ikiwa utakosa maombi, unaweza kuwa na kila aina ya mipango, mifumo na programu, lakini hauna nguvu ya kuziendesha. Ni kama kuwa na waya za umeme, lakini hazijaunganishwa na umeme. Hakuna kinachoenda kufanya kazi. Waya zinaweza kuwa katika mpangilio mzuri na taa inaweza kuwa nzuri, lakini hautapata matokeo, kwa sababu hakuna nguvu za umeme. Nguvu ya kanisa la Kikristo ni sala, na kwa mantiki Paulo anasema, “Kwanza kabisa, omba!"
Kisha, anatuambia tuombee nini? Kwanza, “kwa wafalme na wote walio katika mamlaka." Sasa uzoefu wangu ni kwamba watu wengi wanaodai kuwa watu wa Mungu hawaombei wale walio katika mamlaka, achilia mbali kuwaombea kwanza. Ikiwa wewe ni mwepiskopali, nitakwambia kwamba katika kitabu chako cha maombi kuna sala kwa wale walio katika mamlaka. Ni jambo zuri ipo. Lakini nitakuambia jambo lingine kutoka kwa uzoefu wa kibinafsi kama Muangilikana. Ni jambo moja kusema sala, na jambo lingine kuomba. Vitu hivi viwili havifanani. Watu wengi husema vitu kutoka kwenye kitabu cha maombi na ukiwauliza dakika tano baadaye walichosema, hawawezi kukumbuka. Ni kawaida tu.
Je! Ni mada gani ya kwanza ya sala? “Wote walio katika mamlaka”: rais, maseneta, wawakilishi, magavana, Meya, makamishna wa polisi, wote. Je! Unawaombea? Je ni lini umemwombea rais mara ya mwisho? Je! Ni nini umefanya mwisho - kukosoa au kusali? Ikiwa unaombea watu walio katika mamlaka, utakuwa na kukosoa kidogo. Mungu hakukuita ukosoe, alikuita uombe. Ikiwa hauombi, wewe si mtiifu. Mimi ni mwananchi tu, lakini ninamwombea rais karibu kila siku. Mke wangu ni shahidi. Tunaomba pamoja, na hakuna siku ambayo hatuombei kiongozi wa taifa. Nina uhakika kuwa anahitaji maombi, na maoni yangu ni kwamba Rais wako wa sasa anajua kuwa anahitaji maombi. Je! Tunapaswa kuomba nini kuhusiana na walio kwenye mamlaka? Ni maelezo ya mantiki zaidi ya maombi ambayo naweza kupata mahali popote kwenye Biblia. Katika sehemu ya pili ya aya ya 2 tunaambiwa tuombe “ili tuishi maisha ya utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.” Kwa maneno rahisi: “serikali nzuri." Je! Haungekubaliana na hilo? Ikiwa tunataka kuishi maisha ya utulivu na ya amani katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu, lazima tuwe na serikali nzuri.
Katika aya ya tatu Paulo anaendelea, "Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu." Je! Jambo hili "inamaanisha nini?" Kwa kifungu kilichotangulia, " ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu." - kwa ufupi, “ili tuwe na serikali nzuri.”
Kwanini Mungu anataka utulivu na amani na serikali nzuri? Kwa sababu halisi na ya kweli. Kwa sababu Yeye anatamani watu wote waokolewe na kuingia katika ujuzi wa ukweli. Ni katika hali gani inakuwa rahisi kuleta ukweli kwa watu wote? Chini ya serikali ambayo ni ya haki na usawa na inatunza sheria na utaratibu na uhuru wa raia? Au chini ya serikali ambayo haiwezi kudhibiti vurugu na machafuko na sio ya haki na niya udikteta? Je! Ni serikali ya aina gani hufanya iwe rahisi kuleta ukweli kwa watu wote? Mtu yeyote mwenye busara atajibu: serikali nzuri. Ndio maana Mungu anataka serikali nzuri, kwa sababu inasaidia kueneza injili, ambayo ni kusudi lake katika wakati huu. Hakuna chochote kigumu, hakuna kitu kisichoeleweka, ni busara na hekima.
Koda: TL-L801-100-SWA